Hospitali ya Wilaya ya Kondoa

Mapato ya hospitali yaboresha huduma za maabara

Posted on: September 29th, 2019

Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kondoa imekarabati jengo la maabara hali iliyopelekea kuboreshwa kwa huduma za vipimo katika hospitali hiyo.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri  Dkt. Eusebi Kessy alipokuwa akiongelea ukarabati wa maabara hiyo ofisini kwake hivi karibuni.

 Alisema kuwa ukarabati huo umefanyika kwa kutumia fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya hospitali yatokanayo na uchangiaji wakati wa kutoa huduma mbalimbali hospitalini hapo.

 “Ukarabati huu umefanyika katika maeneo matano ikiwemo kubadilisha muundo wa jengo kutoka wodi hadi muundo wa maabara, kujenga eneo la wagonjwa kusubiria majibu, kusogeza huduma ya vyoo katika jengo hilo kwa ajili ya wagonjwa,kujenga mfumo wa maji safi na maji taka na kubadilisha mfumo wa umeme.”Alisema Dkt.Kessy

Aidha aliongeza kuwa ukarabati huo umepelekea kuongezeka kwa baadhi ya vipimo ambavyo hapo awali havikuwepo ikiwa ni pamoja na kupima kifua kikuu kwa vina saba ambapo mashine ilikuwepo na ilikuwa haitimiki ikiwa ni sambamba na kuanzisha kipimo cha uoteshaji wa vijidudu ambavyo vitapelekea kupatikana kwa majibu sahihi na kwa wakati sahihi na kuongeza mapato ya hospitali.

Kwa upande wake msimamizi wa maabara hiyo Daud Maswaga alisema kuwa wagonjwa wamefurahia maboresho yaliyofanyika kwani awali walikuwa wakipata shida kukaa kwenye jua na kunyeshewa na mvua msimu wa mvua.

“Lakini pia kwa upande wa vipimo tumeboresha tumeongeza vifaa vya kupimia ambavyo vilikuwa vikihitaji sehemu salama lakini pia uboreshaji huu umeongeza usalama kwa wataalam wa maabara na kupunguza hatari ya kupata maambukizi”. Alisema Maswaga

Mmoja wa wagonjwa aliyekuwa akisubiria huduma katika maabara Bi.Fransisca Haule alisema kuwa wanafurahia maboresho yaliyofanyika na kuomba uongozi kuboresha na maeneo mengine ili wananchi wapate huduma bora.