Public Health Education
1.Ugonjwa wa Ebola ni nini?
Ugonjwa utokanao na kirusi cha Ebola ni ugonjwa hatari wenye uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90. Shirika la afya duniani, WHO katika tovuti yake inasema kwa mara ya kwanza ulibainika mwaka 1976 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan. Chanzo cha kirusi hiki hadi sasa hakijulikani lakini popo aina ya (Pteropodidae) wanaonekana kuwa wabebaji wa kirusi hicho,kwa mujibu wa ushahidi uliopo sasa.
2. Binadamu anaambukizwa vipi kirusi cha Ebola?
Mlipuko wa sasa huko Afrika Magharibi kwa kiasi kikubwa umesababishwa na maambukizi ya binadamu kwa binadamu. Maambukizi hutokea pindi mtu anapoambukizwa kupitia sehemu wazi ya mwili wake majimaji ya mgonjwa wa Ebola. Mathalani matapishi, choo, mate, mbegu za kiume, au Semen na damu. Maambukizi yanaweza kutokea pia iwapo ngozi yenye uwazi ya mtu asiye na ugonjwa huo itakumbwa na maji maji yenye kirusi yaliyomo kwenye nguo chafu za mgonjwa, mashuka au sindano zilizotumika.
Zaidi ya wahudumu 100 wa afya wamekumbana na mazingira yenye majimaji kutoka mwili wa mgonjwa wa Ebola pindi wanapokuwa wanatoa huduma kwa wagonjwa hao. Hii hutokea iwapo hawana mavazi stahili ya kujikinga au hawakuzingatia taratibu za kujikinga pindi wanapohudumia wagonjwa. WHO inataka watoa huduma afya katika ngazi zote iwe hospitali, kliniki,zahanati au vituo vya afya wapatiwe taarifa juu ya ugonjwa wa Ebola, unavyoambukizwa na wazingatia mbinu za kuzuia kuenea kwake.
WHO haishauri familia au jamii kuhudumia wagonjwa wanaoweza kuwa na dalili za Ebola majumbani mwao. Badala yake wanataka wapate huduma hospitali au kituo cha afya. WHO imesema maambukizi mengine yameripotiwa kwenye mazishi au mila za mazishi. Katika shughuli hizo waombolezaji wanagusana na mwili wa marehemu na hivyo kujiweka hatarini. WHO inasihi mazishi ya waliofariki dunia kwa Ebola yafanyike kwa kiwango kikubwa cha kujikinga kwa kuvaa mavazi maalum na wanaofariki dunia wazikwe mara moja. Mazishi hayo yafanyike chini ya usimamizi wa wataalamu wa afya.
Mtu anaweza kuambukiza kirusi cha Ebola iwapo damu yake au majimaji ya mwilini yana kirushi hicho. Hivyo basi, wagonjwa wa Ebola wanapaswa kuwa chini ya uangalizi wa hali ya juu kutoka kwa wataalamku na wafanyiwe uchunguzi kuhakikisha kirusi hakipo tena mwilini kabla ya kurejea nyumbani.
Mtaalamu wa afya baada ya kipimo anabaini kuwa mgonjwa ni salama kurejea nyumbani kwa kuwa amepona na hana tena kirusi, hawezi kuambukiza wengine.Hata hivyo wanaume ambao wamepona ugonjwa huo bado wanaweza kuambukiza kupitia njia ya kujamiiana ndani ya wiki saba baada ya kupono. Hivyo wanashauriwa kutoshiriki tendo hilo ndani ya wiki saba baada ya kupona. Na iwapo atalazimika basi ni lazima atumie mpira wa kiume.
3. Nani yuko hatarini zaidi?
Wakati wa mlipuko, walio hatarini zaidi kuambukizwa ugonjwa wa Ebola ni:
- Wahudumu wa afya;
- Wanafamilia au watu wengine walio karibu na mgonjwa wa Ebola
- Waombolezaji ambao wanashika maiti ya mgonjwa wa Ebola kama sehemu ya ibada ya mazishi.
4. Dalili za Ebola ni zipi?
Homa ya ghafla, uchovu wa kina, maumivu ya misuli, maumivu ya kichwa, koo kukauka. Hii hufuatiwa na kutapika, kuhara, vipele, figo kushindwa kufanya kazi, halikadhalika ini, na wakati mwingine damu kuanza kuvunja ndani na nje ya mwili.
Baada ya dalili hizo kuonekana, ugonjwa unaweza kubainika kati ya siku Mbili hadi 21 na hapo ndipo mgonjw anaweza kuambukiza wengine. Wakati ugonjwa haujabainika, mtu hawezi kuambukiza mtu mwingine. Thibitisho la ugonjwa huu hupatikana maabara pekee.
5. Je kuna tiba au chanjo?
Kwa sasa hakuna dawa au chanjo iliyosajiliwa kutibu ugonjwa wa kirusi cha Ebola. Hata hivyo dawa kadhaa zinaendelezwa na WHO imeridhia tiba ya majaribio kutumika kutibu wagonjwa.
read moreUmuhimu wa chanjo
Ukweli kwa familia na kwa jamii kuhusu chanjo
Chanjo huokoa maisha ya hadi watoto milioni 3 kila mwaka.
Chanjo hukinga maradhi, ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwa ni pamoja na surua, homa ya ini (hepatitisi B), dondakoo, kifaduro, nimonia, polio, kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, rubela na pepopunda.
Watoto waliopata chanjo huwa wamekingwa dhidi ya magonjwa haya hatari, ambayo kwa kawaida huweza kusababisha ulemavu au kifo. Watoto wote wana haki ya kupata kinga hii.
Kila msichana na kila mvulana anapaswa kupata chanjo kamili. Kinga utotoni ni muhimu sana
Chanjo kwa mtoto katika mwaka wake wa kwanza na katika mwaka wa pili ni muhimu sana.
Ni muhimu pia kwa kina mama wajawazito kupata chanjo ya pepopunda ili kujikinga wao wenyewe na watoto wao wanaozaliwa.
Pamoja na kwamba kuna maendeleo mazuri ya utoaji chanjo kwa watoto katika miaka iliyopita , katika mwaka 2013 kiasi cha watoto wachanga milioni 21.8 duniani kote hawakuweza kupata huduma za kawaida za chanjo; kiasi ambacho ni karibu nusu ya maisha ya watu katika nchi 3 : India, Nigeria na Pakistan.
Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu sababu za umuhimu wa chanjo, ratiba ya chanjo inayotumika na mahali chanjo inakotolewa kwa watoto.
Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu kuwa kutoa chanjo kwa mtoto mgonjwa kidogo au mwenye ulemavu au mwenye upungufu wa lishe ni salama.
Ukweli kwa ajili ya familia na jamii kuhusu chanjo
- Chanjo ni jambo la lazima. Kila mtoto ni lazima apate chanjo zote zilizopendekezwa. Kinga ya utotoni ni muhimu sana; chanjo katika mwaka wa kwanza na wa pili zina umuhimu wa pekee. Wazazi wote au walezi wengine wanapaswa kuzingatia ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu muda wa kukamilisha chanjo zinazohitajika.
- Chanjo hutoa kinga dhidi ya magonjwa mengi hatarishi. Mtoto ambaye hajapata chanjo yuko katika hatari kubwa ya kupatwa na maradhi, ulemavu wa kudumu au hata kupoteza maisha.
- Mama wote wajawazito pamoja na watoto wao wanapaswa kukingwa dhidi ya pepopunda. Hata kama mama aliwahi kupata chanjo kabla , anapaswa kupata ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu kama bado anahitaji kupewa chanjo ya pepopunda.
- Sindano mpya hazina budi kutumika kwa kila mtu anayepata chanjo. Kila mtu anapaswa kudai sindano mpya kwa kila chanjo anayopewa.
- Ugonjwa huweza kuenea haraka watu wengi wanapokuwa wamekusanyika pamoja. Watoto wote wanaoishi katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa , hasa katika mazingira ya wakimbizi au ya watu waliojikusanya kutokana na janga fulani, wanapaswa kupewa chanjo haraka.
- Kadi ya chanjo ya mtoto (au ya mtu mzima) haina budi kuwasilishwa kwa mtoa chanjo kabla ya kutolewa kwa chanjo.
Ini ni kiungo muhimu sana ndani ya miili yetu, hufanya kazi zaidi ya 500 ; moja ya kazi ni kuchuja na kuondoa sumu kutoka kwenye damu.
Kutokana na sababu mbalimbali kama pombe iliyopita kiasi, sumu kwenye damu au maambukizi; ini hupata shida na kuvimba na kushindwa kufanya kazi vizuri. Hii hali huitwa HOMA YA INI au HEPATITIS.
Katika maeneo yetu, bara la Afrika maambukizi ya virusi wa Homa ya ini ndio sababu kuu ya shida kwenye ini. Virusi vya Homa ya ini vipo vya aina 5 (A,B,C,D,E).
Aina mbili za virusi (B na C ) ndio sababu kuu za ugonjwa wa homa ya ini na husambaa kupitia damu na majimaji ya mwili.
Homa ya ini ni sawa janga linaloua kimya kimya kulingana na takwimu za vifo za dunia inakadiriwa Kirusi cha homa ya ini aina ya B pekee huua watu 600,000 hivi kila mwaka.
Kwa wastani zaidi ya watu bilioni mbili, yaani, asilimia 33 hivi ya watu wote ulimwenguni, wameambukizwa virusi vya HBV, na wengi wao hupona baada ya miezi michache. Watu milioni 350 hivi huendelea kuwa na virusi hivyo mwilini, wengi huishi bila dalili na kuendelea kuambukiza watu wengine.
NAMNA GANI UNAWEZA KUAMBUKIZWA VIRUSI VYA HOMA YA INI (B NA C)…….?
Virusi vya homa ya ini B na C husambaa kupitia damu, shahawa au maji maji mengine ya mwili.
Virusi hivi vina uwezo wa kusambaa na kuambukiza mtu mara 100 zaidi ya virusi vya UKIMWI.
Njia hizi husambaza virusi hivi vya homa ya ini..:
- Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
➡️Mama aliye na maambukizi ya Hepatitis B kumuambukiza mtoto wakati wa kujifungua, iwapo hamna juhudi za kitiba za kuzuia maambukizi kuna uwezekano hadi asilimia 90 kwa mama kumuambukiza mtoto. - Kufanya mapenzi na mtu mwenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini
- Kuchangia vifaa vyenye ncha Kali kama sindano hasa kwa watumia madawa ya kulevya au wachora tattoo, miswaki
- Kuongezewa damu ambayo ina maambukizi ya homa ya ini.
NANI YUPO KATIKA HATARI ZAIDI YA KUPATA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA HOMA YA INI?
° Watoto wachanga waliozaliwa na mama aliye na maambukizi ya virusi vya homa ya ini
° Watu wanaofanya biashara ya ngono
°Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao
°Watu wanaojidunga dawa za kulevya
° Mtu mwenye mpenzi ambaye anaishi na maambukizi ya virusi vya homa ya ini
° Wafanyakazi wa sekta ya Afya
° Watu wa familia wenye ndugu anayeishi na maambukizi ya kudumu ya virusi vya homa ya ini
°Wagonjwa wa figo wanaotumia huduma za kusafisha damu (dialysis)
UGONJWA WA VIRUSI VYA HOMA YA INI HUJA NA DALILI MBALIMBALI…..
Dalili za muda mfupi (acute hepatitis)
➡️ Dalili hizi za mwanzo hutokea ndani ya miezi 6 baada kuambukizwa virusi vya homa ya ini, hutokea kwa baadhi ya watu hazitokei kwa kila mtu.
- Mgonjwa mwenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini hujiskia kuumwa
- Hupoteza hamu ya kula
- Kichefuchefu na kutapika
- Mwili kuuma
- Mkojo kuwa na rangi iliyokolea kama Coca-Cola
- Kupata manjano kwenye macho, vinganja vya mikono/kucha au mwili mzima.
Kwa nini ni muhimu kupima ili kujua kama una maambukizi ya virusi vya homa ya ini? ….
Watu wengi huishi na maambukizi ya virusi vya homa ya ini bila kufahamu. Kwa kawaida katika kipindi fulani cha maisha mtu 1 kati ya watu 3 huambukizwa virusi vya homa ya ini. Baada ya kuambukizwa, kuna kundi la watu hubaki na maambukizi ya kudumu ya virusi vya homa ya ini ambayo huwa hayana dalili yoyote na kuendelea kuua ini kimyakimya. Dalili huja kuonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa. Huonekana wakati tayari ini limenyauka au lina kansa.
Hivyo Mtu aliye na maambukizi ya kudumu ya virusi vya homa ya ini aina B akianza matibabu mapema, anaweza kuzuia ini lake lisiharibike sana. Pia kwa wenye maambukizi ya virusi aina C matibabu ya dawa wiki 12 humaliza virusi vyote.
Nani yupo katika hatari ya maambukizi ya Ini
- Watu wanaoishi kwenye maeneo yenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini kwa zaidi ya asilimia 2. -Tanzania ni moja ya nchi zenye kiwango cha maambukizi ya virusi vya homa ya ini kwa wastani wa 5% hivyo watanzania wote ni muhimu kupima
- Watu wote wanaotumia dawa za kulevya na kujidunga
- Wafanyakazi katika sekta ya afya
- Watu wote wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI
- Watu wote ndani ya familia wanaoshi na ndugu aliyeambukizwa virusi vya homa ya ini
- Watu wote wanaotumia dawa za kufubaza kinga ya mwili (immunosuppressive therapy)
- Watu wote wenye ugonjwa wa figo wanahitaji kuanza dialysis
- Kina mama wajawazito wote
- Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao.
Makundi ambayo ni lazima kupatiwa chanjo ya homa ya ini
- Watoto wote
- Watu wote wanaotumia dawa za kulevya na kujifungua
- Watu wote wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI
- Watu wote ndani ya familia wanaoshi na ndugu aliyeambukizwa virusi vya homa ya ini
- Watu wote wanaotumia dawa za kufubaza kinga ya mwili (immunosuppressive therapy)
- Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao
- Watu wote wanaoufanya biashara ya ngono
- Watu wote ambao wana mpenzi zaidi ya mmoja ndani ya miezi 6
- Watu wenye maradhi ya kudumu ya ini
- Watu wengine wote wanahitaji KUJIKINGA dhidi ya virusi vya homa ya ini
Malaria ni ugonjwa unaoathiri watu wengi sana duniani. Malaria husababisha vifo vya watu milioni 2.7 duniani kote, ambapo vifo vingi hutokea barani Afrika. Ugonjwa wa malaria huonekana katika nchi 100 duniani kote.
Kwa Tanzania, mikoa ambayo inaongoza kwa maambukizi ya malaria ni Kagera (41.1%), Lindi (35.5%), Mtwara (36.6%), Mwanza (31.4%), Mara (30.3%). Mikoa ambayo maambukizi ya malaria ni kidogo ni Manyara (1%), Kilimanjaro (1%) na Dar-es-salaam (1.2%). Kwa Zanzibar, maambukizi ya malaria ni kwa asilimia 0.8.
Malaria huonekana sana katika kanda ya Tropiki. Ugonjwa huu wa malaria uligunduliwa mwaka 1880 na Charles Louis Alphonse Laveran, katika hospitali ya jeshi ya Constatine, Algeria, baada ya kuona vimelea vya plasmodium, kutoka kwa mgonjwa aliyefariki kwa ugonjwa huo.
Malaria ni kati ya magonjwa ya maambukizi ambao husababishwa na vimelea vya Plasmodium, ambavyo humfikia binadamu kupitia kung’atwa na mmbu aina ya Anopheles jike.
Kuna aina 5 za vimelea viletavyo malaria:
- Plasmodium falciparum - Hupatikana sana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara. Asilimia 75 ya wagonjwa wote wa malaria barani Afrika husababishwa na vimelea hivi. Mwaka 2006, kati ya watu milioni 247 duniani waliougua malaria, asilimia 91 walisababishwa na vimelea hivi (Afrika 98%) na kusababisha vifo kwa asilimia 90 mwaka huo huo barani Afrika.
- Plasmodium malariae - Pia hupatikana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara, Asia ya Mashariki, Indonesia na katika visiwa vya magharibi mwa Pacific. Kati vya vimelea vyote vya malaria, plasmodium malariae ndio huonekana kwa uchache zaidi.
- Plasmodium ovale - Hupatikana Afrika Magharibi, Ufilipino, Mashariki mwa Indonesia, Papua New Guinea, Cambodia, Bangladesh, India, Thailand na Vietnam.
- Plasmodium vivax - Huonekana katika bara la Marekani, Latin Amerika na baadhi ya sehemu za bara la Afrika.
- Plasmodium knowlesi - Hupatikana katika bara la Asia ya mashariki katika nchi za Bormeo, Myanmar, Malaysia, Ufilipino, Singapore na Thailand. Haipatikani katika bara la Afrika.
Mzunguko wa maisha ya vimelea vya malaria
Mwenyeji wa msingi ya vimelea vya malaria ni mbu aina ya anopheles wa kike, ambae pia ni msambazaji, na binadamu ni mwenyeji wa kati. Mbu anapokuwa anajipatia chakula kwa kunywa damu kwa kuuma binadamu mwenye maambukizi ya vimelea vya malaria, ndio mzunguko wa kwanza huanza, ambapo gametocyte za vimelea vya plasmodium hugawanyika ndani ya mbu na kutengeneza gametocyte za kike na za kiume na baada ya hapo gametocyte hizo za kike na za kiume, hujiunga ndani ya mfumo wa chakula wa mbu na kutengeneza Ookinete ambayo hupenyeza kwenye kuta za mfumo wa chakula na kutengeneza Oocyst nje ya ukuta wa mfumo wa chakula, na hapo hupasuka na kutengeneza Sporozoites na kuhamia kwenye tezi za mate za mbu, na kuwa tayari kuambukiza binadamu mwengine pindi mbu anapojitafutia chakula.
Kwa mbu jike damu ndio lishe yake wakati dume lishe yake ni nekta ya mimea, hivyo mbu dume hasambazi ugonjwa huu. Na mbu jike aina ya anopheles hupenda kujipatia lishe kipindi cha usiku.
Maambukizi ya malaria yanaweza kupatikana kwa kuongezewa damu ingawa ni nadra sana.
Kwa Binadamu pindi anapong’atwa na mbu hupata maambukizi kupitia mate ya mbu, na vimelea vya plasmodium kwenye hatua ya sporozoites huingia kwenye damu na kuelekea kwenye ini ambapo hutengeneza schizonts na baadae schizonts hupasuka na kuachia merozoites kuelekea kwenye damu na kutengeneza immature trophozoite kiataalamu zinajulikana kam ring stage ambapo baada ya hapa huwa kuna hatua mbili tofauti zinazofuata,hatua ya kwanza ni mature trophozoites na kutengeneza schizont nyingine kwenye damu na vilevile schizont hii hupasuka na kutoa immature trophozoites na kuendelea kujirudia tena hatua hii. Hatua nyingine ni gametocyte ambayo hubebwa na mbu.
Dalili za ugonjwa wa malaria
- Homa
- Maumivu ya kichwa
- Kichefuchefu
- Kutapika
- Maumivu ya misuli
- Manjano
- Degedege
- Kupoteza fahamu
- Kukua kwa wengu
- Dalili za mwanzo hutokea kati ya siku 10 hadi wiki 4, na dalili nyingi hutokea pale hatua ya merozoites inapoachiwa nyingi kwenye damu baada ya schizonts kupasuka.
Madhara ya ugonjwa malaria
- Malaria ya kichwa (cerebral malaria)
- Matatizo ya kupumua (pulmonary edema)
- Viungo kushindwa kufanya kazi (organ failure)
- Upungufu wa damu
- Upungufu wa sukari mwilini (hypoglycemia)
- Shinikizo la chini la damu (hypotension)
- Haemoglobinuria
- Disseminated intravascular coagulopathy
- Metabolic acidosis
Vipimo na uchunguzi
- Kipimo cha damu na kutumia hadubini
- Thin film--hutumika kutambua aina ya vimelea vya plasmodium (falciparum,ovale,vivax,malariae)
- Thick film---hutumika kutambua idadi ya vimelea/µL
- Kipimo cha damu bila kutumia hadubini
- Malaria Rapid Diagnostic Test
- PCR
Matibabu
- Dawa za malaria
- Mstari wa kwanza (dawa mseto)
- Artemether plus Lumefantrine
- Dihydroartemisinin plus Piperaquine
- Mstari wa Pili
- Amodiaquine
- Mstari wa tatu
- Quinine
- Mstari wa kwanza (dawa mseto)
- Dawa za kushusha homa na maumivu
- Paracetamol
Kama sehemu ya tiba, mgonjwa anashauriwa pia kula na kunywa maji ya kutosha.
Jinsi ya kuzuia maambukizi ya Malaria
- Kuzuia mazalio ya mbu
- Fyeka vichaka na ondoa madimbwi ya maji katika maeneo yanayokuzunguka.
- Kuzuia kung’atwa na mbu
- Matumizi ya vyandarua vyenye dawa ya kuua mbu
- Matumizi ya dawa za kupulizia za kuua mbu majumbani
- Matumizi ya dawa za kupaka za kuua mmbu
- Dawa za kuzuia malaria kwa wasafiri watokao nchi sizizo na malaria
- Proguanil
- Malarone
- Mefloquine
- Dawa za kuzuia malaria kwa kina mama wajawazito (IPT)
- Sulfadoxine Pyrimethamine (SP) hutolewa kwa kina mama katika wiki ya 20 na wiki ya 36 ya ujauzito.