Hospitali ya Wilaya ya Kondoa

Umuhimu wa Chanjo

Posted on: October 15th, 2019

Umuhimu wa chanjo

Ukweli kwa familia na kwa jamii kuhusu chanjo

Chanjo huokoa maisha ya hadi watoto milioni 3 kila mwaka.

Chanjo hukinga maradhi, ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwa ni pamoja na surua, homa ya ini (hepatitisi B), dondakoo, kifaduro, nimonia, polio, kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, rubela na pepopunda.

Watoto waliopata chanjo huwa wamekingwa dhidi ya magonjwa haya hatari, ambayo kwa kawaida huweza kusababisha ulemavu au kifo. Watoto wote wana haki ya kupata kinga hii.

Kila msichana na kila mvulana anapaswa kupata chanjo kamili. Kinga utotoni ni muhimu sana

Chanjo kwa mtoto katika mwaka wake wa kwanza na katika mwaka wa pili ni muhimu sana.

Ni muhimu pia kwa kina mama wajawazito kupata chanjo ya pepopunda ili kujikinga wao wenyewe na watoto wao wanaozaliwa.

Pamoja na kwamba kuna maendeleo mazuri ya utoaji chanjo kwa watoto katika miaka iliyopita , katika mwaka 2013 kiasi cha watoto wachanga milioni 21.8 duniani kote hawakuweza kupata huduma za kawaida za chanjo; kiasi ambacho ni karibu nusu ya maisha ya watu katika nchi 3 : India, Nigeria na Pakistan.

Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu sababu za umuhimu wa chanjo, ratiba ya chanjo inayotumika na mahali chanjo inakotolewa kwa watoto.

Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu kuwa kutoa chanjo kwa mtoto mgonjwa kidogo au mwenye ulemavu au mwenye upungufu wa lishe ni salama.

Ukweli kwa ajili ya familia na jamii kuhusu chanjo

  1.  Chanjo ni jambo la lazima. Kila mtoto ni lazima apate chanjo zote zilizopendekezwa. Kinga ya utotoni ni muhimu sana; chanjo katika mwaka wa kwanza na wa pili zina umuhimu wa pekee. Wazazi wote au walezi wengine wanapaswa kuzingatia ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu muda wa kukamilisha chanjo zinazohitajika.
  2.  Chanjo hutoa kinga dhidi ya magonjwa mengi hatarishi. Mtoto ambaye hajapata chanjo yuko katika hatari kubwa ya kupatwa na maradhi, ulemavu wa kudumu au hata kupoteza maisha.
  3.  Mama wote wajawazito pamoja na watoto wao wanapaswa kukingwa dhidi ya pepopunda. Hata kama mama aliwahi kupata chanjo kabla , anapaswa kupata ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu kama bado anahitaji kupewa chanjo ya pepopunda.
  4.  Sindano mpya hazina budi kutumika kwa kila mtu anayepata chanjo. Kila mtu anapaswa kudai sindano mpya kwa kila chanjo anayopewa.
  5.  Ugonjwa huweza kuenea haraka watu wengi wanapokuwa wamekusanyika pamoja. Watoto wote wanaoishi katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa , hasa katika mazingira ya wakimbizi au ya watu waliojikusanya kutokana na janga fulani, wanapaswa kupewa chanjo haraka.
  6.  Kadi ya chanjo ya mtoto (au ya mtu mzima) haina budi kuwasilishwa kwa mtoa chanjo kabla ya kutolewa kwa chanjo.