Waaswa kuwapeleka watoto kupata chanjo
Posted on: October 22nd, 2019
Wanawake na walezi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi na watoto wao wa kuanzia umri wa miezi tisa hadi miaka mitano katika vituo vyote vya afya ili kuhakikisha wanapata chanjo ya Surua Rubela na Polio inayoendelea kutolewa.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota alipokuwa akizindua zoezi la utoaji wa chanjo hizo katika Hospitali ya Mji Kondoa hivi karibuni.
“Mjitokeze kwa wingi kwasababu chanjo hii ni muhimu sana kwa watoto wetu na inasaidia kupunguza gharama za matibabu hapo baadae kwani mtoto anakuwa ameshapata kinga,”alisema Mhe. Makota.
Awali akisoma taarifa ya zoezi Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt. Florence Hilary alisema kuwa Halmashauri imejipanga kutoa chanjo ya polio kwa watoto 5052 na chanjo ya Surua Rubela kwa watoto 8590.
Zoezi la utoaji chanjo linaendeshwa nchi nzima kwa siku tano kuanzia tarehe 17/10/2019 na linatarajia kukamilika tarehe 21/10/2019 na limebeba kauli mbiu ya “Chanjo ni Kinga kwa pamoja Tuwakinge.”