Hospitali ya Wilaya ya Kondoa

Wizara ya Afya yawapongeza HeadInc

Posted on: September 29th, 2019

Wizara ya Afya imelipongeza Shirika la Head Inc lenye Diaspora wa Kondoa kutoka nchini Marekani kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika masuala ya afya.

Pongezi hizo zimetolewa na Dkt. Dorothy Gwajima kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati wa ufunguzi wa zoezi la kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Kondoa zitakazotolewa na madaktari bingwa kutoka shirika hilo.

“Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha huduma za afya kila siku na wenzetu hawa Diaspora wameliona hilo na wakaona ni vema kuunga mkono jitihada hizo kwa kuja kutoa huduma hii nyumbani tunawashukuru sana na naamini mnaweza kusaidia katika maeneo mengine kwa kutoa elimu kwa wataalam wetu wa afya.”Alisema Dkt. Gwajima

Aliongeza kuwa kuna michakato mingi hadi walipofika Kondoa hasa maeneo ya bandarini na katika Taasis zingine za serikali ili kuingiza vifaa vyenu lakini hilo linafanyika katika kuhakikisha kuwa dawa na vitu vingine vinakuwa katika ubora na viwango vinavyotakiwa nchini na kuahidi kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuanzisha dawati litakalokuwa

 linashughulikia masuala ya Diaspora na kupunguza michakato hiyo.

“Nashauri uongozi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji kutengeneza Mpango Mkakati wa kuboresha huduma za Afya na kuwapatia wenzetu hawa ili wakifika huko Marekani wanaweza kuona jinsi ya kutusaidia ikiwemo kuboresha huduma za wagonjwa mahututi.”Alishauri Dkt. Gwajima

Akiongea katika ufunguzi huo Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota aliwashukuru wadau hao kwa msaada walioutoa na kuwasihi wananchi kutumia fursa hiyo kwa kuwataarifu wengine na kujitokeza kwa wingi kwani zoezi hilo ni kama lililofanyika mwaka jana na litawasaidia wananchi kuondokana na maradhi.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa Msoleni Dakawa akitoa salamu za shukrani alisema kuwa ujio wa Diaspora hao umetokana na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli katika upande wa Afya ambapo pia ametoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Kingale.

Ujio wa Diaspora katika Halmashauri ya Mji Kondoa umewezeshwa na shirika la Head Inc kutoka nchini Marekani ambapo watatoa huduma ya afya katika Hospitali ya Mji Kondoa kwa muda wa siku nne kwa magonjwa ya kinywa na meno,magonjwa ya kinamama,magonjwa ya watoto na magonjwa ya macho.